Askofu wa Jimbo Katoliki la Embu, Mhashamu Peter Kimani Ndung’u, amewataka Wakristo na viongozi wa kisiasa kudumisha amani, upendo na unyenyekevu, akionya dhidi ya kauli na vitendo vinavyoweza kuleta migawanyiko katika jamii.
Akihutubia waamini wakati wa Misa ya kuadhimisha miaka 40 ya Jimbo Katoliki la Embu katika Kanisa Kuu la Watakatifu Petro na Paulo, Askofu Kimani aliwataka viongozi kuwa waangalifu na kauli zao, akisema maneno makali yanaweza kusababisha uhasama na maumivu katika familia.
Alilaani visa vya watu kujeruhiwa, kupoteza maisha na mali kuharibiwa kutokana na vurugu, huku akiwataka wananchi kubaki na umoja kama familia moja, jimbo, kaunti na taifa.
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Isiolo, Mhashamu Peter Makau Munguti, aliwataka Wakristo kuishi imani yao kupitia matendo na kuwa mashahidi wa upendo.
Askofu Makau pia alikemea unyanyasaji wa majumbani, ukosefu wa ajira, ugumu wa kiuchumi, ukosefu wa haki na ukosefu wa uvumilivu wa kisiasa, akiwataka wanandoa kutatua migogoro kwa amani na kuepuka kutumia nguvu.