Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji, amesema viongozi wa eneo hilo watahamasisha wachungaji na maaskofu kuandaa maombi katika uwanja wa Nembure, kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa Jumamosi.
Mukunji amesema hawataruhusu uwanja huo kutumiwa kuwagawa wananchi, kuchochea chuki au kusababisha mauaji. Amehimiza viongozi kutumia mikutano ya kisiasa kuleta umoja na amani miongoni mwa wakazi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Runyenjes, Muchangi Karemba, amesema mikutano ambayo inalenga kuwagawa wananchi katika uwanja huo haitaruhusiwa.
Kauli za viongozi hao zinajiri baada ya ghasia kuzuka Nembure Stadium Jumamosi, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha.
Viongozi wamewataka wananchi kukataa kuchochewa kisiasa na kusisitiza umuhimu wa kulinda amani katika kaunti ya Embu.