Papa Mtakatifu Leo XIV ametoa wito wa kuimarishwa kwa heshima ya binadamu huku akieleza uungwaji mkono wake kwa juhudi za kufutwa kwa adhabu ya kifo nchini Marekani na duniani kote.
Katika ujumbe wa video uliotolewa Aprili 24 kwa waliohudhuria maadhimisho ya miaka 15 tangu kufutwa kwa adhabu ya kifo katika jimbo la Illinois, yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha DePaul nchini Marekani, Papa Leo amesema Kanisa linafundisha kuwa heshima ya mtu haipotei hata baada ya kufanya makosa makubwa.
Alieleza kuwa alijiunga na washiriki kusherehekea uamuzi huo wa kihistoria wa mwaka 2011, akisisitiza kuwa anaunga mkono wote wanaopigania kukomeshwa kwa adhabu ya kifo duniani.
Papa Leo XIV aliongeza kuwa anaomba juhudi hizo zisaidie kuongeza utambuzi wa heshima ya kila mtu na kuwahamasisha wengine kuunga mkono azma hiyo ya haki.
Akizungumzia masuala ya haki, Papa alisisitiza kuwa inawezekana kufanikisha haki bila kutumia adhabu ya kifo. Alibainisha kuwa mifumo madhubuti ya kuwashikilia wahalifu inaweza kulinda jamii bila kuwanyima kabisa nafasi ya kujirekebisha.
Alikumbusha pia msimamo wa Papa Francis pamoja na watangulizi wake, kwamba ustawi wa jamii na utekelezaji wa haki vinaweza kupatikana bila kuhitaji adhabu ya kifo.
Aidha, alinukuu Katekisimu ya Kanisa Katoliki inayofundisha kuwa adhabu ya kifo haikubaliki kwa kuwa ni shambulio dhidi ya heshima na utu wa mwanadamu.
Kwa kuhitimisha, Papa alisisitiza umuhimu wa kulinda uhai kuanzia kutungwa kwa mimba hadi kifo cha asili, akisema haki ya kuishi ndiyo msingi wa haki nyingine zote za binadamu, na kwamba jamii inalinda maisha ndipo inaweza kustawi na kufanikiwa.