Askofu Obanyi aonya vijana dhidi ya kutumiwa vibaya kisiasa

Askofu Joseph Obanyi Sagwe wa Jimbo Katoliki la Kakamega ametoa onyo kali kwa vijana dhidi ya kuruhusu kutumiwa vibaya na wanasiasa, akisisitiza umuhimu wa kusimama imara katika maadili na kufanya maamuzi yenye busara.
Akihubiri wakati wa Misa ya Vijana iliyofanyika Mumias, Askofu Obanyi alieleza masikitiko yake kuhusu mwenendo mpya wa wahuni unaozidi kushika kasi, ambapo vijana wanahamasishwa kushiriki vitendo vya vurugu kwa manufaa ya wanasiasa. Aliwataka vijana kukataa kushiriki katika vitendo hivyo na badala yake kuwa mfano bora katika jamii.
Kuhusu haki ya kupiga kura, Askofu alisisitiza kuwa ni “dhambi” kwa mtu mwenye sifa zote, haki na kitambulisho halali kushindwa kupiga kura. Alieleza kuwa kushiriki katika uchaguzi ni wajibu wa kila raia na njia muhimu ya kuleta mabadiliko chanya katika taifa.
Aidha, aliwaonya vijana dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, akibainisha kuwa uraibu huo unaharibu mustakabali wao na kudhoofisha jamii kwa ujumla. Aliwataka kuchagua njia sahihi za maisha na kujiepusha na mienendo inayoweza kuwaangamiza.
Katika hotuba yake, Askofu Obanyi pia aliikosoa serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Aliitaka serikali kuwajibika na kuacha “kucheza na akili za wananchi,” akisisitiza kuwa wananchi wanastahili kuona matokeo ya ahadi zinazotolewa.
Kuhusu elimu, Askofu aligusia mfumo wa elimu wa CBE (Competency-Based Education), akisema wazazi wamechoshwa na kile wanachokiona kama majaribio yanayoendelea hata baada ya miaka kumi. Alitaka tathmini ya kina ifanyike ili kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha wanafunzi ipasavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *