Walimu wa Junior Secondary School (JSS) katika Kaunti ya Meru wameipa serikali hadi tarehe 1 Mei kuwapatia kandarasi za ajira, wakitegemea maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa yaliyosema kuwa kuwaajiri walimu kwa mfumo wa ufunzwa kazini (internship) ni kinyume cha sheria.
Wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa KUPPET Kaunti ya Meru, Muthoni Njira, walimu hao wamesema kuwa mgomo wao bado unaendelea na hawatarejea kazini hadi madai yao yatakapotekelezwa.
Wameeleza kuwa mfumo wa ufunzwa kazini hauwapi haki stahiki za ajira na unakiuka sheria za kazi.
Aidha, walimu hao wanataka shule hizo za junia zitenganishwe rasmi na shule za msingi na kupewa uongozi kamili, ukiwemo mwalimu mkuu pamoja na naibu wake, ili kuboresha usimamizi na utoaji wa elimu.
Walimu hao sasa wanaitaka serikali kuchukua hatua za haraka kushughulikia suala hilo kabla ya muda walioweka kufika.