Wakazi wa Embu wapinga mpango wa kituo cha karantini ya Ebola

Baadhi ya wakazi wa Kaunti ya Embu wameeleza kupinga mpango wa serikali wa kuanzisha kituo cha karantini ya ugonjwa wa Ebola, wakidai kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha afya na usalama wa wananchi.

Wakazi hao wanasema serikali inaonekana kutanguliza maslahi yake kuliko yale ya wananchi. Wamedai kuwa badala ya kuleta wagonjwa wa Ebola nchini, serikali inapaswa kuimarisha mikakati ya kuzuia magonjwa hatari kuingia nchini na kuboresha huduma za afya kwa Wakenya.

Aidha, baadhi yao wamehoji uwezo wa taifa katika kukabiliana na magonjwa ya kawaida, wakisema kuwa kuhusishwa na ugonjwa hatari kama Ebola kunaweza kuongeza changamoto katika sekta ya afya.

Wakazi hao pia wamekosoa wabunge kwa kile walichokitaja kuwa kushindwa kutetea maslahi ya wananchi waliowachagua. Wengine wameeleza wasiwasi kuhusu usalama wa wahudumu wa afya watakaohusika na kuwahudumia wagonjwa hao.

Hata hivyo, wametoa wito kwa serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu mpango huo na hatua zilizowekwa kuhakikisha usalama wa wananchi na wahudumu wa afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *